TUMAINI KATIKA UPEO WA MACHO
Biblia imejaa matumaini. Mtume Paulo hasa ni mtume wa matumaini. Anaandika kwa kanisa la Rumi, anawatia moyo kwa maneno haya, "kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi, ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini" Warumi 15:4. Sura ya 15 inahitimisha na maneno haya: " Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu". Wakati siku zijazo zinapoonekana kuwa na mashaka, Neno la Mungu hujaza mioyo yetu kwa tumaini.
Paulo akimwandikia Tito katika Tito 2:13 anamthibitishia kudumu " ukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na mwokozi wetu.
Historia ilikuwa na mahali pa kuanzia na itakuwa na mahali pa kuishia. Ilianza Mungu alipoimba dunia hii, na upeo wa uumbaji ni kurudi kwa Bwana wetu, ambaye hatimaye ataumba upya mbingu mpya na nchi mpya.
Kuna matukio 3 makubwa katika Biblia: uumbaji, msalaba, na ujio wa Kristo. Kurudi kwa Bwana katika sayari hii iliyokata tamaa inayotamani sana tumaini ndio upeo wa vizazi vyote. Inaanza kufikia kilele cha onesho la muda mrefu la dhambi na kifo. Manabii wa agano la kale na wanafunzi wa agano jipya waliutangaza. Malaika waliuthibitisha, na Yesu aliuahidi.
Daudi mtunzi wa zaburi kwa shangwe alitangaza "Mungu wetu atakuja wala hatanyamaza, Moto utakula mbele zake, na tufani yavuma sana ikimzunguka pande zote" Zaburi 50:3)
Paulo alirudia maneno hayo alipotamka kwamba "Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza"(1Wathesalonike 4:16), Hata malaika wakati wa kupaa kwa Kristo walithibitisha, wanafunzi walipoinua vichwa vyao na kukaza macho yao kwa Bwana aliyekuwa akipaa, wakiangalia kwa shauku kubwa mbinguni, malaika walisimama kando yao wakisema, " Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni ." (Matendo 1:11). Na hata Yesu mwenyewe aliahidi kwamba atarudi aliposema wazi kwa wanafunzi wake "Nitakuja tena" Yohana 14:3. Ujio wa pili wa Kristo ndilo jibu la mwisho kwa swali kuu la maisha-masuala yale tunayosumbuka nayo ambayo yanaonekana kutokuwa na suluhisho.
Ujio wa pili wa Kristo na maswali makuu ya maisha.
Ujio wa pili wa Kristo ndilo suluhisho la tatizo la upweke, kukata tamaa, kutokuwa na tumaini, na utupu ule unaokera ulio ndani ya mioyo yetu. Ndani kabisa ya moyo wa mwanadamu Kuna hamu ya kupenda na kupendwa. Tuliumbwa ili kupata uzoefu wa upendo usiokuwa na masharti usiotokana na kile tunachokitenda bali na sisi ni nani. Kuna hamu ile ya asili ya kutaka urafiki. Hatukuumbwa tuwe wapweke.
Sote Tunahitaji hisi hii ya kwamba Kuna mtu fulani anajali. Kila mmoja wetu ana hamu hii ya kupendwa bila masharti. Kukubalika kama tulivyo, bila kujali ni wapi tunatoka au kile ambacho tumekitenda wakati uliopita. Ufunuo 21:3 inathibitisha siku moja Yesu anaporudi tutakuwa pamoja na Mungu milele, "Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao". Maskani ya Mungu ni makazi halisi ya Mungu.
Hatukuumbwa ili tuishi mbali na Yeye. Tuliumbwa kwa ajili Yake. Yeye anayetufahamu upeo anatupenda upeo na punde atakuja kutupeleka nyumbani kuishi Pamoja Naye. Tunaweza kutarajia siku njema za usoni kwa ahadi za Mungu - umilele pamoja Naye. Sisi ni vidoa vidogo vya vumbi la dunia katika ulimwengu. Tuliumbwa kwa ajili ya ushirika pamoja na Mungu aliyetuumba. Tuna mahali ambapo ndiyo kwetu. Siku moja tutamwona uso kwa uso na kugubikwa na upendo wake. Kila siku anatamani sana kuwa rafiki yetu.
Siku moja tutaishi katika uwepo wake. Siku moja upendo utatawala juu ya vyote, na mioyo yetu utakuwa na amani. Siku moja hamu iliyoko ndani ya kutaka kupendwa kikamilifu pasipo vikwazo katikati itatoweka. Ujio wa pili wa Kristo si tu jibu la upweke peke yake. Pia ni suluhisho la mwisho wa tatizo la maumivu.
Kutatua tatizo la maumivu
Maumivu, mateso,huzuni na machozi husumbua dunia yetu. Magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani, kisukari na hata Corona yanawatesa mamia ya maelfu ya watu kila siku. Magonjwa ya kila namna huharibu miili yetu vibaya sana. Lakini miili yetu inapoteswa sana kwa maumivu kwa sababu ya magonjwa, bado tunaweza kupata faraja ya kweli katika ukweli kwamba siku moja Yesu atarudi, na maumivu yote na uzuni vitakoma. Yesu atakuja tena anaahidi katika Ufunuo 21:4 kwamba, "Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita." Unapoteseka, mwili wako unapoteseka sana kwa maumivu, pale ambapo huwezi kuvumilia kwa siku moja zaidi, pale ambapo macho yako yamejaa machozi, unaweza kuwa na tumaini tena. Katika dunia ile mpya furaha itakuwa tele, na miili yetu itatikisika kwa mtetemo wa Afya.
Hata mauti nayo itashindwa Mpendwa.
Hivyo unapopitia changamoto fulani basi unapaswa kuangalia ng'ambo ya maumivu yako, na kuona mwisho mwema. Mtume Paulo anarudia maneno haya ya pekee, "......Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa. Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda." (1Wakorintho 15:51-54)
Je umempoteza mpendwa kwa kifo? je umemlaza mtoto kupumzika kando ya mlima fulani wenye nyasi nyingi? Je mke wako, mume wako, mtoto wako wa kiume au wa kiume, amepatwa na ugonjwa fulani wa kufisha? Je huzuni yaonekana kuwa kubwa kiasi cha kutokuweza kuibeba peke yako? Yesu atakukamilisha. Sikiliza sauti yake ikikutia nguvu moyoni mwako. Iko siku bora zaidi inakuja. Unaweza kuwa na tumaini tena. Katika upweke unaweza kuwa na tumaini tena. Katika maumivu na kuvunjwa moyo unaweza kuwa na tumaini tena. Katika udhalimu unaweza kuwa na tumaini tena. Katika machozi unaweza kuwa na tumaini tena. Yesu anakuja na hiyo Ndiyo habari njema kuliko zote ambazo mtu yeyote anaweza kuifikiria.
Hama Hakika Baada ya TAABU kuna mwisho mwema. Mchague Bwana Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako leo.
Hama Hakika Baada ya TAABU kuna mwisho mwema. Mchague Bwana Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako leo.
Mungu akupe tafakari njema ya neno lake.
Ubarikiwe Sana Sana Sana Rafiki.


Comments
Post a Comment